WANANCHI WATAKIWA KUFATILIA TAARIFA MUHIMU HUSUSA HALI YA HEWA INAYOTOLEWA NA MAMLAKA HUSIKA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imetoa wito kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kufuatilia taarifa muhimu, hususan utabiri wa hali ya hewa unaotolewa na mamlaka husika.
Wito huo umetolewa baada ya kamati hiyo kufanya ziara katika Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania jijini Dar es Salaam Machi 16, 2026, ambapo imewahimiza wananchi kufuatilia kwa karibu taarifa muhimu zikiwemo za utabiri wa hali ya hewa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Seleman Kakoso, amesema kufuatilia utabiri wa hali ya hewa humsaidia mwananchi kutambua hali halisi katika shughuli mbalimbali ikiwemo biashara, usafiri majini pamoja na kilimo.
“Unapofuatilia utabiri wa hali ya hewa utatambua uhalisia wa shughuli za kibiashara, hali ya hewa majini na pia shughuli za kilimo kwa wale wanaojishughulisha na kilimo,” amesema.
Ameongeza kuwa baadhi ya Watanzania wana tabia ya kupuuza taarifa muhimu zinazotolewa, ikiwemo tahadhari ya mvua kubwa, hali ambayo wakati mwingine husababisha madhara ambayo yangeweza kuepukika kama wananchi wangezingatia taarifa hizo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Ladslaus Chang'a ameishukuru Serikali kwa kuongeza idadi ya watumishi wa mamlaka hiyo kutoka watumishi 532 mwaka 2022 hadi kufikia watumishi 618 mwaka 2026, hatua aliyosema itaongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za utabiri wa hali ya hewa nchini.



Comments
Post a Comment