TIMU YA WHEEL CHAIR TENNIS YAOMBA MILIONI 40 KUSHIRIKI MASHINDANO NCHINI MOROCCO
Timu ya taifa ya tenesi kwa walemavu yaomba Milioni 40 kushiriki mashindano ya Morocco
DAR ES SALAAM: TIMU ya Taifa ya wachezaji wa tenesi kwa walemavu (Wheelchair Tennis) imeomba msaada wa Shilingi milioni 40 ili kufanikisha safari ya kwenda kushiriki mashindano ya kimataifa yatakayofanyika nchini Morocco kuanzia Machi 30 hadi Aprili 3, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kocha wa timu hiyo ambaye pia ni Katibu, Riziki Salumu, amesema kuwa timu hiyo imejiandaa kikamilifu kushiriki mashindano hayo muhimu ya kimataifa.
Salumu amesema jumla ya watu 10 wanatarajiwa kusafiri, wakiwemo wachezaji wanane, kiongozi mmoja pamoja na msaidizi wake.
Ameeleza kuwa ushiriki wao katika mashindano hayo utasaidia kuitangaza Tanzania kimataifa, pamoja na kuwapa wachezaji fursa ya kupata nafasi za ufadhili endapo watafanya vizuri.
Amesisitiza kuwa bado kuna uelewa mdogo kwa jamii kuhusu mchezo wa tenesi kwa watu wenye ulemavu, hali inayochangia kukosekana kwa sapoti ya kutosha, licha ya juhudi zinazofanywa na wachezaji hao kuiletea nchi heshima kimataifa.
"Gharama za safari hiyo ni Shilingi milioni 50, ambapo hadi sasa wamefanikiwa kukusanya Shilingi milioni 17 tu, na hivyo bado wanahitaji Shilingi milioni 40 ili kukamilisha maandalizi.
Naye nahodha wa timu ya Taifa, Vosta Isaya, amewaomba wadau, mashirika pamoja na Serikali kujitokeza kusaidia timu hiyo ili iweze kushiriki mashindano hayo muhimu.
Mchezaji wa timu hiyo, Pendo James, amesema wameanza maandalizi tangu Januari mwaka huu, akibainisha kuwa mashindano hayo kwa kawaida hufanyika Februari lakini mwaka huu yamesogezwa mbele kutokana na mwezi wa Ramadhani.
Aidha, Jumanne Nasoro amesema mwaka jana timu ya wanawake ilipata udhamini na kushiriki mashindano hayo, lakini timu ya wanaume ilikosa nafasi hiyo.
Hivyo mwaka huu wana matumaini makubwa ya kupata sapoti ili waweze kushiriki, kwani wamejiandaa vya kutosha.
Wachezaji hao wamesema kuwa kutoshiriki mashindano hayo kunaweza kusababisha adhabu ya kutojumuishwa kwa muda katika mashindano yajayo, huku wakisisitiza kuwa michezo ni ajira na chanzo cha kipato, hivyo wanahitaji kuungwa mkono ili kufanikisha ndoto zao.






Comments
Post a Comment