CRDB FINALI NDIO MPANGO TEMBO CARD VISA WASHINDI KWENDA KOMBE LA DUNIA

CRDB Yazindua Kampeni ya “Fainali Ndiyo Mpango” kwa Tembo Card Visa, Washindi Kwenda Kushuhudia Fainali za Kombe la Dunia 2026
Benki ya CRDB Bank imezindua rasmi kampeni maalum iitwayo “Fainali Ndiyo Mpango” kupitia matumizi ya Tembo Card Visa, ikiwa na lengo la kuhamasisha wananchi, wadau na wapenzi wa michezo kutumia malipo ya kidijitali katika kufanya manunuzi na kulipia huduma mbalimbali. Kupitia kampeni hiyo, wateja wa benki hiyo watapata fursa ya kujishindia zawadi mbalimbali ikiwemo safari ya kwenda kushuhudia fainali za mashindano ya FIFA World Cup 2026 zitakazofanyika katika nchi za Marekani, Mexico na Canada kuanzia mwezi Juni hadi Julai mwaka huu.
Akizungumza na vyombo vya habari wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na wa Kati wa CRDB Bank, Bonaventure Paul, amesema kampeni hiyo ni sehemu ya juhudi za benki hiyo kuendelea kuhamasisha matumizi ya malipo ya kidijitali pamoja na kuwazawadia wateja wao kwa uaminifu wao. Amesema mpira wa miguu ni zaidi ya mchezo kwani unaunganisha watu kutoka mataifa mbalimbali bila kujali lugha au tamaduni, hivyo benki hiyo imeona ni fursa nzuri kuwapa wateja wake nafasi ya kuwa sehemu ya msisimko wa mashindano ya FIFA World Cup 2026. “Kampeni hii ni sehemu ya jitihada za kuendeleza malipo ya kidijitali, kuleta ubunifu katika huduma za kifedha na kuwazawadia wateja wetu kwa uaminifu wao. Kupitia Tembo Card Visa wateja watapata urahisi na usalama wa kufanya malipo huku wakipata nafasi ya kushinda zawadi mbalimbali,” amesema Paul. Ameongeza kuwa kampeni hiyo itadumu kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia uzinduzi wake hadi Juni 11 mwaka huu, ambapo droo ya mwisho itachezeshwa siku hiyo. Katika kipindi hicho, wateja wanaotumia Tembo Card Visa, Prepaid Card pamoja na Infinity Credit Card watapata nafasi ya kushinda zawadi mbalimbali endapo watafanya miamala isiyopungua 30 kwa mwezi. Hatua hiyo inalenga kuhamasisha matumizi ya malipo yasiyotumia fedha taslimu ambayo ni muhimu katika kukuza sekta ya fedha nchini. Kwa mujibu wa Paul, jumla ya washindi 20 watapatikana katika kampeni hiyo. Washindi 10 watapata safari ya kwenda kushuhudia mechi za FIFA World Cup 2026 huku washindi wengine 10 wakijishindia zawadi za vifaa vya kielektroniki ikiwemo runinga ya kisasa ya inchi 85 pamoja na kisimbuzi. Amefafanua kuwa droo ya kwanza itachezeshwa Aprili 12 ambapo washindi wanne watapata nafasi ya kusafiri kwenda Marekani kushuhudia mechi za Kombe la Dunia, huku washindi watatu wakijishindia runinga na kisimbuzi. Droo ya pili itafanyika Mei 12 ambapo washindi watatu watapata safari ya kwenda Canada na wengine watatu kushinda runinga pamoja na kisimbuzi. Droo ya mwisho itafanyika Juni 11, siku ambayo pia itakuwa hitimisho la kampeni hiyo, ambapo washindi saba watapatikana; watatu watasafiri kwenda Canada kushuhudia mechi za Kombe la Dunia huku washindi wanne wakijishindia runinga na kisimbuzi. Benki hiyo imewataka wateja na wapenzi wa michezo kutumia kikamilifu Tembo Card Visa katika manunuzi yao ya kila siku ili kuongeza nafasi ya kushinda zawadi hizo, ikiwemo safari ya kipekee ya kwenda kushuhudia fainali za FIFA World Cup 2026 pamoja na zawadi nyingine za kuvutia.

Comments

Popular posts from this blog

MATAIFA 8 KUIMBA TAMASHA LA PASAKA

PIMEA USIKU WA WANA NDOA ULIVYOFANA MSIFICHANE NA KUWEKEANA VITU

UONGOZI DHAIFU VYATAJWA KUVURUGA TAASISI ZA VIJANA