VIJANA WAHIMIZWA KUTUMIA FURSA ZA UCHUMI WA KIJANI KUJIKWAMUA KIUCHUMI

Vijana Wahimizwa Kuchangamkia Fursa za Uchumi wa Kijani Mkurugenzi wa CRDB Bank Foundation, Tuliesther Mwambapa, ametoa rai kwa vijana nchini kuendelea kuchangamkia fursa zinazotolewa na taasisi mbalimbali ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza Machi 17, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kutangaza matokeo ya programu ya uhamasishaji wa ubunifu wa vijana katika uchumi wa kijani, Mwambapa amesema taasisi hiyo itaendelea kuwasaidia vijana kifedha na kitaalamu ili kukuza biashara zao na kuchangia maendeleo ya taifa. Ameeleza kuwa programu hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya CRDB Bank Foundation na wadau mbalimbali, wakiwemo taasisi za maendeleo pamoja na mashirika ya kimataifa yanayojihusisha na masuala ya mabadiliko ya tabianchi. Amesema ushirikiano huo umewezesha kuanzishwa kwa mifumo ya kidijitali inayorahisisha upokeaji na uchambuzi wa maombi.
Akizungumzia uzinduzi wa programu hiyo uliofanyika Februari 12 jijini Dodoma, Mwambapa amesema tukio hilo lilihudhuriwa na viongozi wa serikali akiwemo Waziri wa Mipango na Uwekezaji, ambaye alifungua rasmi dirisha la maombi kwa vijana na wajasiriamali nchini kote. Aidha, ameipongeza serikali kwa kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kushiriki katika kukuza uchumi jumuishi na endelevu, akisisitiza kuwa juhudi hizo zinachangia kuwainua vijana kiuchumi kupitia ubunifu na ujasiriamali.
Mwambapa amesema programu hiyo inalenga makundi matatu ya vijana ambayo ni wamiliki wa biashara changa, wajasiriamali wadogo pamoja na wanafunzi wenye mawazo ya biashara, kwa lengo la kuwasaidia kubuni suluhisho za changamoto za kimazingira huku wakijipatia kipato. Amebainisha kuwa ndani ya mwezi mmoja tangu kufunguliwa kwa dirisha la maombi, jumla ya maombi 3,967 yalipokelewa kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Ameongeza kuwa hatua inayofuata ni tathmini ya kitaalamu ya miradi iliyowasilishwa, itakayofanywa na jopo la wataalamu kutoka taasisi mbalimbali, ambapo washiriki watakaofaulu watapatiwa mafunzo maalum kabla ya kufanyiwa uhakiki wa biashara zao.

Comments

Popular posts from this blog

MATAIFA 8 KUIMBA TAMASHA LA PASAKA

PIMEA USIKU WA WANA NDOA ULIVYOFANA MSIFICHANE NA KUWEKEANA VITU

UONGOZI DHAIFU VYATAJWA KUVURUGA TAASISI ZA VIJANA