BALOZI ZENA AWAHIMIZA WAFADHILI KUWEKEZA MISAADA INAYOBADILI MAISHA

Balozi Zena Ahmed Said Awahimiza Wafadhili Kuwekeza Misaada Inayobadili Maisha. DAR ES SALAAM: Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Balozi Mteule (Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Saudi Arabia), Mhandisi. Zena Ahmed Said, amewahimiza wafadhili kutoka ndani na nje ya Tanzania kuelekeza misaada yao kwenye miradi yenye tija na inayoweza kubadili maisha ya wahitaji kwa muda mrefu, badala ya misaada ya muda mfupi kama chakula na mavazi pekee.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya Iftar Gala iliyoandaliwa na Taasisi ya SETTA (Social Economic Tier of Turkish Alumni) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uturuki nchini Tanzania, Balozi Zena amesema uwekezaji katika sekta muhimu kama elimu, miradi ya kiuchumi na fursa za maendeleo ni njia bora ya kupunguza changamoto zinazowakabili watu wenye uhitaji.
Amesisitiza kuwa misaada ya aina hiyo ina uwezo wa kuleta mabadiliko ya kudumu katika maisha ya jamii na kusaidia kujenga msingi imara wa maendeleo. “Uwekezaji katika elimu, miradi ya kiuchumi na fursa za maendeleo unaweza kusaidia kumaliza changamoto zinazowakabili wahitaji kwa muda mrefu,” amesema.
Aidha, Balozi Zena amesema huu ni wakati mwafaka kwa Uturuki na wadau wengine wa maendeleo kuongeza juhudi za kusaidia Watanzania wenye uhitaji, hususan katika kipindi hiki cha Ramadhani na Kwaresma, ili kuhakikisha msaada unaotolewa unakuwa na manufaa ya kudumu kwa jamii.
Kwa upande wake, Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Dkt. Bëkir GEZËR, amesema lengo la hafla hiyo lilikuwa kuwakutanisha wahitimu wa Kitanzania waliosoma nchini Uturuki pamoja na wadau mbalimbali ili kuimarisha ushirikiano wa kielimu na kijamii.
Ameeleza kuwa tukio hilo pia linalenga kuimarisha mtandao wa mahusiano kati ya wahitimu hao na taasisi mbalimbali kwa ajili ya kuendeleza ushirikiano katika nyanja tofauti za maendeleo. Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mgeni Rasmi Mhandisi Zena Ahmed Said, ambaye pia ni Balozi mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Saudi Arabia, pamoja na Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Dkt. Bëkir Gezer, na wahitimu mbalimbali wa vyuo vya Uturuki wanaoishi Tanzania.

Comments

Popular posts from this blog

MATAIFA 8 KUIMBA TAMASHA LA PASAKA

PIMEA USIKU WA WANA NDOA ULIVYOFANA MSIFICHANE NA KUWEKEANA VITU

UONGOZI DHAIFU VYATAJWA KUVURUGA TAASISI ZA VIJANA