CRDB YATOA BILIONI 2.3 KWA WATEJA KUPITIA KAMPENI YA SIMBANKING

CRDB Yatoa Bilioni 2.3 kwa Wateja Kupitia Kampeni ya SimBanking
DAR ES SALAAM Benki ya CRDB imetenga jumla ya shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya zawadi kwa wateja wake watakaofanya miamala na malipo kupitia huduma ya SimBanking, ikiwa ni sehemu ya kampeni maalum ya kuhamasisha matumizi ya huduma za kifedha za kidijitali. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya SimBanking Kimpango Wako, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo, amesema kuwa katika kampeni hiyo mshindi wa kwanza wa droo ya mwisho atajipatia shilingi milioni 30, huku mshindi wa pili akipata milioni 20 na wa tatu milioni 10.
Amesema mbali na fedha taslimu, washindi wengine watajishindia zawadi mbalimbali ikiwemo safari za kwenda nje ya nchi, kutembelea mbuga za wanyama, vocha za manunuzi pamoja na vifaa kama simu za mkononi na kompyuta mpakato. “Kampeni hii inalenga kuwapa motisha wateja pamoja na watoa huduma kutumia zaidi mifumo ya kidijitali katika miamala yao ya kifedha,” amesema Nshekanabo. Aidha, ameeleza kuwa zawadi hizo zitatolewa kupitia droo zitakazokuwa zikifanyika kila wiki, kila mwezi pamoja na droo za kila robo mwaka, ili kuongeza nafasi kwa washiriki wengi kushinda. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wateja wa Awali na Wakati wa benki hiyo, Bonaventure Paul, amesema kuwa wateja watakaofanya miamala mbalimbali kupitia SimBanking ikiwemo malipo ya huduma, uhamishaji fedha na manunuzi ya kila siku watapata nafasi ya kushiriki na kushinda katika kampeni hiyo.

Comments

Popular posts from this blog

MATAIFA 8 KUIMBA TAMASHA LA PASAKA

PIMEA USIKU WA WANA NDOA ULIVYOFANA MSIFICHANE NA KUWEKEANA VITU

UONGOZI DHAIFU VYATAJWA KUVURUGA TAASISI ZA VIJANA