KAMATI YA BUNGE YAIOMBA SERIKALI KUPANUA ENEO LA JKCI KUIMARISHA HUDUMA
Kamati ya Bunge yaiomba Serikali kupanua Eneo la JKCI na Kuimarisha Huduma za Afya Nchini
DAR ES SALAAM
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Jamii imeitaka Wizara ya Afya kuhakikisha Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (Jakaya Kikwete Cardiac Institute – JKCI) inapatiwa eneo kubwa zaidi ili iweze kupanua huduma zake na kuwahudumia wananchi wengi zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 14, 2026, Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Mbunge wa Hai/Meru Magharibi Johaneth Lukumai amesema baada ya kamati kutembelea hospitali hiyo imebaini umuhimu wa taasisi hiyo kupanuliwa ili kuongeza uwezo wa utoaji wa huduma za matibabu ya moyo.
Amesema pamoja na kuongeza eneo, pia kuna haja kwa JKCI kuendelea kujitanua na kusogeza huduma zake katika mikoa mbalimbali nchini ili wananchi waweze kupata huduma za afya kwa wakati bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kufika Dar es Salaam.
Aidha, Lukumai alibainisha kuwa bado kuna changamoto katika utekelezaji wa baadhi ya mifumo ya ufadhili wa huduma za afya, ikiwemo masuala yanayohusiana na mifuko ya bima ya afya, ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi ili kuboresha huduma kwa wananchi.
Pia aliiomba Serikali kuipatia JKCI kibali maalum cha kununua dawa zake moja kwa moja ili kurahisisha upatikanaji wa dawa muhimu kwa wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika taasisi hiyo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya Florence Samizi aliwataka wananchi kuwa na utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara ili kugundua mapema magonjwa na kupata matibabu kwa wakati.
“Wananchi wasisubiri hadi waumwe ndiyo wakimbilie hospitali. Ni muhimu kuwa na utaratibu wa kupima afya mara kwa mara ili kujua hali ya afya zao na kupata matibabu mapema,” amesema Samizi.




Comments
Post a Comment