MWAKA MMOJA WA MEMBE




Ni mwaka mmoja sasa tangu kutokea kifo cha mwanasiasa mkongwe,Bernard Membe ambapo leo familia yake imefanya misa maalum ya kumbukumbu katika Kanisa la Mtakaifu Joseph Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya Misa hiyo maalum, Mjane wa Marehemu Membe, Dorcas Richard amesema kikubwa anachoomba kwa marafiki wa Membe ni kuendelea umoja, upendo na mshikamano aliowaachia marehemu.
“Tarehe rasmi aliyofariki Mzee ni kesho Mei 12, familia ilipanga tufanye misa kijijini alikopumzishwa mzee, lakini kutokana na changamoto za miundombinu na mvua ndio maana tumeamua kuifanya ibada hii hapa St Joseph, lakini na kule kijiji ibada maalum kama hii inaendelea.”amesema Dorcas na kuongeza
Amesema “familia tunawashukuru watu wote walioshiriki na sisi katika kipindi chote cha msiba, wamekuwa bega kwa bega na sisi  hadi katika kuandaa misa hii maalum ya mwaka mmoja, tunaomba ushirikiano huu uendelee, upendo, mshikamano uendelee kuwepo kati ya marafiki, ndugu na jamaa,”amesema
Aidha, amesema kama familia wapo kwenye mchakato wa kuanzisha taasisi maalum kwa ajili ya kuenzi mchango wa marehemu Bernard Membe.



Kwa upande wake Waziri wa Habari , Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema wamekuwa na siku nzuri ya kutafakari kazi nyingi alizozifanya Hayati Membe nchini hasa katika jimbo la Mtama ambapo ndipo alipozaliwa.
“Tumeandaa Misa kwaajili ya kumkumbuka kaka yetu Bernard Membe ambapo kesho Tarehe 12 atakuwa anatimiza mwaka mmoja tangu afariki, tumekuwa na siku nzuri ya kutafakari kazi nyingi alizozifanya katika nchi yetu, katika jimbo la Mtama alipozaliwa”
“Kuna mambo aliyaanzisha na hapa ndiyo ilikuwa tafakari kubwa, kuna mambo aliyaanzisha kwa kanisa ambalo alikuwa akihudumiwa ikiwemo baadhi ya ujenzi wa makanisa na majengo mbalimbali ya kanisa, ambapo tumekubaliana tuangalie namna ambayo tutazikamilisha Zile ndoto alizozianzisha”
Nape amesema kwa upande wa Mtama, Hayati Membe alikuwa ni muumini wa kubadilisha maisha ya watu kwani wakati wa uongozi wake alikuwa akitamani kila mtu awe na maisha mazuri.
“Alitamani mtu aishi kwenye nyumba nzuri, apate maji safi, na hizi ndizo ndoto ambazo nimeendelea nazo, ndiyo maana tangu aliponiacha tumehakikisha tumesambaza umeme jimbo zima, tumepeleka maji kila mahali, mawasiliano, shule,”amesema Nape na kuongeza
“Na katika kijiji na kata aliyotoka wakati anaondoka hakukuwa na sekondari, hivyo tumejenga sekondari na tukaipa jina lake Benard Membe ili kumkumbuka kuwa alikuwa ni mtu ambaye alipenda kubadilisha maisha ya watu anaowaongoza,”amesema.
Nae Alex Msama ambae ni rafiki wa familia akimzungumzia marehemu Membe amesema wanamshukuru Mungu kwa maisha ya Membe aliyokua amemjalia hadi pale alipomchukua Mei 12, 2023 na kwamba kama marafiki na taifa kuna mengi ambao amewaachia.
“Kwa sisi watu wake wa karibu hatuna budi kuendeleza umoja aliyotuachia siku zote alisisitiza hili, tusameheana tunapokoseana, tusiwe watu wa visasa, tuwe wakweli na kuwa wazalendo, tusiwe  na umimi, tuinue wenzetu ili kupiga hatua kutoka sehemu moja au nyingine na zaidi tusimamie kile tunachokiamini.
“Kikubwa alichotuachia Membe ni kusimamia  kile unachoona ni sahihi kwa ajili ya kulinda na uhifadhi utu wako, kuwa jasiri war oho, hicho ndicho Membe alikisimamia,”amesema. 
Membe alifariki siku ya Ijumaa Mei 12, 2023, majira ya saa tano za asubuhi, taarifa ya kifo cha mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania, kutoka Chama cha Mapinduzi, (CCM), ndipo zilipoanza kusambaa kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.
Amefariki asubuhi katika hospitali ya Kairuki, Mikocheni jijini Dar es Salaam, baada ya kupelekwa alfajiri ya siku hiyo kutokana na changamoto ya kifua.

Comments

Popular posts from this blog

MATAIFA 8 KUIMBA TAMASHA LA PASAKA

PIMEA USIKU WA WANA NDOA ULIVYOFANA MSIFICHANE NA KUWEKEANA VITU

UONGOZI DHAIFU VYATAJWA KUVURUGA TAASISI ZA VIJANA