WIKI YA AZAKi 2024 YAZINDULIWA KUJIKITA DIRA YA MAENDELEO
Wananchi wamehimizwa kupaza sauti zao kikamilifu katika kutoa maoni yatakayosaidia upatikanaji bora wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society (FCS), Justice Rutenge baada ya uzinduzi rasmi wa Wiki ya asasi za kiraia nchini (AZAKi 2024) itakayofanyika jijini Arusha kuanzia Septemba 9 hadi 13, 2024 ambapo zaidi ya washiriki 500 watahusika.
Maadhimisho ya wiki hiyo yamebeba kaulimbiu ya "sauti, maono na thamani" ikilenga kuwa, licha ya tofauti ya mitazamo na makundi, bado sauti zetu zinapaswa kuwa kitu kimoja ili kurahisisha mchakato wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Ameongeza kuwa, Wiki ya AZAKi mwaka huu inafanyika mapema Septemba, tofauti na ilivyozoeleka awali kila ifikapo Oktoba tangu kuanzishwa kwake 2018, lengo likiwa ni kuhamasisha wananchi kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa.
Kwa upande wake, Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation, Sandra Oswald, amesema imekuwa rahisi kushirikiana na FCS kuelekea Wiki ya AZAKi kutokana na kaulimbiu ya mwaka huu kuendana na dhima ya taasisi hiyo kuwa chachu ya maendeleo ya jamii kupitia elimu, afya na teknolojia.
Katika wiki ya AZAKi 2024, kati ya mambo yatakayojadiliwa ni pamoja na njia zinazoweza kuleta thamani halisi na chanya kwa kufikia maono ya pamoja ya mustakabali wa nchi na kuimarisha ushirikiano baina ya sekta binafsi, umma, na asasi za kiraia




Comments
Post a Comment