UMOJA WA MABALOZI KUKUTANA MIAKA 61
UMOJA wa Mabalozi wa Nchi za Afrika wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini wameandaa Maadhimisho ya miaka 61 ya Siku ya Afrika yatakayoadhimishwa matukio makubwa matatu.
Matukio hayo ni Mbio za Mabalozi wa Afrika zikatazofanywa keshokutwa mjini Dar es Salaam na kuwashirikisha mabalozi wa nchi hizo,watumishi wa ofisi za ubalozi,watumishi wa wizara inayowahudumia na wadau wengine.
Hayo yalibainishwa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ali Bujiku katika mkutano na waandishi wa habari akiambatana na baadhi ya mabalozi wa nchi hizo.
Alisema tukio la pili kati ya matukio hayo matatu ni kutoa msaada kwa shule nne za Dar e Salaam zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum na tukio la tatu la maadhimisho hayo ni viongozi hao na wadau wengine kushiriki maonesho ya vyakula vya kiafrika katika Hoteli ya Serena Dar es Salaam Mei, 20 mwaka huu.
Balozi Bujiku alisema Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni ‘Kujenga mifumo ya elimu thabiti kwa ajili ya kuongeza ufikiaji wa mafunzo jumuishi yenye ubora barani Afrika,.
Alisema Siku ya Afrika huazimishwa Mei 25, kila mwaka ambayo awali ilijulikana kama Siku ya Uhuru wa Afrika, iliyoanza kuadhimishwa mwaka 1963 baada ya kuundwa wa Umoja wa Nchi za Afrika(OAU)na baadaye Umoja wa Afrika(AU).
Alisema wakati wa uundwaji wake nchi 32 tu za Afrika ndizo zilikuwa na uhuru lakini sasa nchi zote 55 ziko huru na kwamba malengo ya kuundwa kwake yalikuwa ni kusaidia nchi ambazo hazijapata uhuru za Afrika zipate lakini sasa lengo lao ni kuendelea kuuimarisha umoja wao na kusisitiza ushirikiano.
Katika kutekeleza azma yao, kwenye tukio la mbio za mabalozi, wanatarajia washiriki zaidi ya 700 kushiriki mbio hizo wakiwemo wanariadha mashuhuru nchini, mabalozi, wafanyakazi wa ubalozi,wizara na wadau wengine na hadi sasa zaidi ya washiriki 300 wameshathibitisha kushiriki.
Mbio hizo ni za kilometa tano na 15 na zitaanza saa 12 kamili asubuhi Jumamosi wiki huu katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere ,Dar es Salaam(JNICC) kuelekea OysterBay kupitia Daraja la Tanzanite na kurudi JNICC.
Akizungumzia matukio yote matatu katika maadhimisho hayo, Kiongozi wa Mabalozi nchini, Balozi wa Comoro,Dk Ahamada El Badaoui alisema wamechagua kufanya matukio hayo kwa lengo kugusa jamii na kuinua kiwango cha elimu kwa wote.
“Tutatoa misaada kwa wanafunzi katika shule nne zilizo na wanafunzi wenye mahitaji maalam ili kuwasaidia kufikia ndoto zao kielimu,”alisema Balozi Dk El Badaoui .
Balozi wa Morocco nchini, Zakaria El Goumiri alisema katika maadhimisho hayo atakimbia mbio za Kilometa 15 yeye na watumishi wengine wa ubalozi huo na lengo ni kuonesha umoja, mshikamano wa Afrika.
“Tumaadhimisha Siku ya Afrika kwa kuonesha kwa vitendo umoja wetu, kusaidia jamii na kuimarisha ushirikiano, tunataka tuoneshe uwezo wetu wa kuendelea kushikamana,”alisema Balozi Goumiri.
Balozi wa Kenya nchini,Isack Njenga alisema wanaungana katika kuadhimisha siku hiyo kwa kushiriki riadha, kusaidia jamii na maonesho ya vyakula vya mataifa ya Afrika ili kuendelea kuuimarisha umoja wa nchi hizo.

Comments
Post a Comment