NaCONGO KUFANYA UCHAGUZI WA VIONGOZI
Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) limetangaza mchakato wa uchaguzi wa wajumbe na viongozi wa Baraza hilo, utakaofanyika kuanzia Mei 21 hadi Juni 26, 2024.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti Kamati ya Mpito ya Kuratibu Uchaguzi wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Christina Kamili Ruhinda, ameyatangazia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na umma kwa ujumla kuhusu kuanza kwa mchakato wa Uchaguzi wa Baraza, pamoja na ratiba na taratibu muhimu za kuzingatiwa ili kufanikisha mchakato mzima wa Uchaguzi huo.
Ruhinda amebainisha ratiba ya uchaguzi huo, ambapo amesema mchakato wa uchaguzi ngazi ya Wilaya utafanyika kuanzia Tarehe 21 hadi 29 Mei, 2024. Mchakato wa uchaguzi ngazi ya Mkoa utafanyika Tarehe 3 hadi 11 Juni, 2024 na mchakato wa uchaguzi ngazi ya Taifa utafanyika kuanzia Tarehe 14 hadi 26 Juni, 2024.
Aidha, Ruhinda ameeleza kuwa, wagombea wa nafasi mbalimbali katika Baraza hilo, sharti wakidhi vigezo ambapo taratibu zote za kuchukua fomu za kugombea zimeaninishwa katika tovuti ya Baraza hilo kwa anwani ya www.nacongo.or.tz na barua pepe ya kurudisha fomu ni uchaguzinacongo@gmail.com.
Uchaguzi huo unajiri kufuatia Baraza lililopo madarakani kumaliza muda wake wa miaka mitatu mapema Juni 30, 2024 ambapo uchaguzi wake ulifanyika Juni, 2021. NaCoNGO ni chombo huru cha mwamvuli wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yaliyosajiliwa Tanzania Bara kisheria.

Comments
Post a Comment