WANANCHI WATAKIWA KUJIKINGA NA SHINIKIZO LA DAMU
Wananchi wametakiwa kuchukua hatua za mapema za kinga, uchunguzi na matibabu ya ugonjwa wa shinikizo la juu la damu ili kupunguza madhara yanayosababishwa na ugonjwa huo ambao umeendelea kuwa tishio kubwa kwa afya ya jamii.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Shinikizo la Juu la Damu Duniani, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge amesema kuwa kila mwaka ifikapo Mei 17 dunia huadhimisha siku hiyo kwa lengo la kuongeza uelewa wa jamii kuhusu ugonjwa wa shinikizo la juu la damu.
Amesema maadhimisho ya mwaka 2026 yanabeba kaulimbiu isemayo: “Kudhibiti Shinikizo la Damu kwa Pamoja: Pima shinikizo lako la damu mara kwa mara, ushinde ugonjwa huu unaoua kimyakimya.”
Kwa mujibu wa Dkt. Kisenge, kaulimbiu hiyo inalenga kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya jamii, familia, sekta ya afya pamoja na wadau mbalimbali katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Ameeleza kuwa shinikizo la juu la damu ni hali inayotokea pale nguvu ya msukumo wa damu ndani ya mishipa inapokuwa kubwa kuliko kiwango kinachotakiwa, hali inayoufanya moyo kufanya kazi kwa nguvu zaidi kusukuma damu kwenda katika viungo muhimu vya mwili kama ubongo, figo, macho na mishipa ya damu.
“Ugonjwa huu hujulikana kama muuaji wa kimya kimya kwa sababu unaweza kuendelea kwa muda mrefu bila kuonesha dalili za wazi,” amesema.
Hata hivyo amesema baadhi ya wagonjwa wanaweza kupata dalili kama maumivu ya kichwa, kuona kiza, maumivu ya shingo, kutoka damu puani, kupoteza fahamu au kupata kiharusi.
Aidha, amesema ugonjwa huo unaweza kumpata mtu wa umri wowote, wakiwemo watoto.
Dkt. Kisenge amesema kuna aina kuu mbili za shinikizo la damu. Aina ya kwanza ni shinikizo la damu la asili ambalo huchangia asilimia 90 hadi 95 ya wagonjwa na mara nyingi halina sababu inayoeleweka moja kwa moja. Aina ya pili ni shinikizo la damu linalotokana na magonjwa mengine kama matatizo ya figo, mishipa ya damu au mfumo wa homoni.
Ametaja vihatarishi vya ugonjwa huo kuwa ni pamoja na historia ya ugonjwa katika familia, uzito mkubwa kupita kiasi, matumizi ya chumvi nyingi, kutofanya mazoezi, uvutaji wa sigara, matumizi makubwa ya pombe, ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi pamoja na ongezeko la umri.
JKCI imeeleza kuwa kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu afya zao ni sehemu muhimu ya kupunguza mzigo wa magonjwa ya moyo nchini. Kaulimbiu ya “Jua Namba Zako” inalenga kujenga utamaduni wa wananchi kujitambua kiafya mapema kwani hatua ndogo ya kupima afya leo inaweza kuokoa maisha kesho.
Pia wananchi wamehimizwa kufanya mazoezi mara kwa mara, kula lishe bora yenye matunda na mboga mboga, kupunguza matumizi ya chumvi na mafuta mengi, kuacha uvutaji wa sigara, kupunguza matumizi ya pombe pamoja na kupima afya mara kwa mara.
Kwa wagonjwa wanaotumia dawa za shinikizo la damu, wametakiwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya, kutumia dawa kwa usahihi na kutositisha matumizi ya dawa bila ushauri wa kitabibu.
“Kupima shinikizo la damu mara kwa mara ni hatua rahisi lakini muhimu inayoweza kusaidia kugundua ugonjwa mapema, kuanza matibabu kwa wakati na kuzuia madhara makubwa yanayoweza kuzuilika,” amesema Dkt. Kisenge.





Comments
Post a Comment