ZUCHU KUSAIDIA WASANII CHIPKIZI 300 "ZUCHU iMBEJU MASTERCLASS 2026
DAR ES SALAAM:MSANII wa muziki wa Bongo Fleva Zuchu ametangaza rasmi mpango maalum wa mafunzo kwa wasanii chipukizi unaojulikana kama “Zuchu iMbeju Masterclass 2026”, utakaowahusisha wasanii 300 kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Mpango huo unatarajiwa kuanza rasmi Juni 16, 2026 ukiwa na lengo la kuinua vipaji vya vijana pamoja na kuwajengea uwezo wa kunufaika kiuchumi kupitia sanaa wanazozifanya kila siku.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika makao makuu ya crdbbank.co.tz, Zuchu amesema kuwa programu hiyo imeandaliwa kwa kushirikiana na foundation.crdbbank.co.tz kupitia mpango wa iMbeju, ikiwa ni sehemu ya kusaidia vijana wenye vipaji nchini Tanzania kupata elimu na ujuzi wa kukuza kazi zao za kisanii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa CRDB Foundation, Tully Esther Mwambapa, amesema washiriki watakaopata nafasi ya kujiunga na mafunzo hayo watapatiwa elimu mbalimbali ikiwemo namna ya kujitangaza, kusimamia vipaji vyao na kutumia sanaa kama chanzo cha kipato cha kudumu.
Aidha, Mwambapa ameeleza kuwa maombi ya kushiriki yatafanyika kupitia mfumo wa Fursa Hub kwa kutembelea tovuti ya CRDB Bank Foundation na kufuata maelekezo ya usajili.
Amesema washiriki 10 wa kwanza kujisajili watagharamiwa ada ya mafunzo hayo na benki hiyo, huku washiriki wengine wakitakiwa kuchangia kiasi cha shilingi 500,000 ili kupata nafasi ya kushiriki.
Mafunzo hayo yataanza Juni 16, 2026 na yatafanyika katika ofisi za makao makuu ya CRDB Bank.





Comments
Post a Comment