FAINI NI MUHIMU ZINAPASWA KUHESHIMIWA
RAIS wa Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki, Fauz Twaib amesema fani ya sheria ni muhimu katika taifa lolote hivyo inapaswa kuheshimiwa.
Twaib amesema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika Siku ya Taaluma ya Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ( UDSM).
"Umuhimu wa uanasheria na kuwepo kwa wanasheria ndiyo inayofanya fani hii kuwa muhimu.
"Wanasheria tuna nafasi muhimu katika maisha ya binadam hivyo tutumie vizuri nafasi hiyo kwa kufanya yale ambayo jamii inahitaji tufanye. Tuna wajibu wa kijamii wa kuwekeza kutumia kile tulichonayo," amesema.
Pia Twaib alielezea uzoefu wake katika fani hiyo, ambapo alisema alianzia kazi ya ualimu katika shule ya msingi, akajiendeleza na kuwa mhadhiri wa sheria UDSM.
baadaye alikuwa wakili kisha akateuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu na sasa ni Rais wa Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki.
Naye Mratibu wa Masomo ya Degree ya Awali kutoka Shule Kuu ya Sheria UDSM, Dk Florencia Kimario alisema katika siku hiyo wanafunzi wanakutana na watu mbalimbali kutoka kwenye sheria, uwakili, jaji, polisi na watunga sheria kutoka mihimili mbalimbali ya serikali.
"Pia tunaalika kampuni za uwakili zinasaidia kifedha pia zinasaidia kuwafundisha kwa vitendo wanafunzi hawa wa sheria," amesema.
Amesema lengo la kuwa na siku hiyo ni kuwatia moyo wanafunzi wanaosomea sheria, pamoja na kuwaeleza changamoto watakazoweza kukutana nazo ili wajiandae kisaikolojia.
"Ni siku ambayo walimu wa sheria wanakaa na wanafunzi wao na kuzungumza nao, kusikiliza kutoka kwao kujua kile wanachofundisha changamoto ziko wapi, nini kiongezwe," amesema.


Comments
Post a Comment